250. Baba Uliye Mbinguni

1.  Baba uliye mbinguni 

    tunakuomba kwa mioyo.

    Twakuomba kama wana

    waombavyo baba zao,

    twaamini: Baba yetu 

    watusikia mbinguni.

 

2.  Jina lako litakaswe 

    likitangazwa popote, 

    walisikiao Neno

    walifuate kwa bidii. 

    Tulitumie vizuri 

    Jina la Mungu Mwenyezi.

 

3.  Na ufalme wako uje 

    kwa mataifa mengine. 

    Tupe roho na rehema  

    tuzishike amri zako. 

    Ufalme wako ukae 

    katika mioyo yetu.

 

4.  Utakayo yatimizwe 

    duniani kama mbinguni.

    Shetani, mwili, dunia,

    wasituzuie sisi,

    kuyatenda mambo mema 

    na kukutii mpaka kufa. 


5.  Utupe leo chakula 

    chetu cha kututunzia,

    tupate afya, chakula, 

    mavazi, mali, na jamaa, 

    serikali ya amani, 

    tutakushukuru Baba.


6.  Tuondolee makosa 

    yasitusumbue tena,

    tulivyowaondolea 

    na waliotukosea. 

    Tuwasaidie kama 

    unavyotusaidia. 


7.  Usituingize sisi 

    majaribuni popote. 

    Shetani asidanganye

    na kutushinda kwa hila. 

    Ila tukijaribiwa

    tushinde kwa nguvu  zako.

 

8.  Tuokoe maovuni 

    yoyote, Bwana, yalivyo, 

    ya mwili hata ya moyo 

    ya mali na ya heshima; 

    mwisho tutakapokufa, 

    tufe tukitengemana. 


9.  Kwani wako ni ufalme 

    nguvu nao utukufu

    hata milele hakuna 

    vinavyokushinda wewe.

    Kwa Jina la Mwana wako

    kubali maombi yetu. 


10. Ameni! Yatafanyika 

    yote tuliyokuomba. 

    Utaitika: Ameni, 

    tukikuomba kwa moyo. 

    Ameni ni kuambiwa: 

    “yatafanyika kwa kweli!” 

Comments

Popular posts from this blog

276. Nina Haja Nawe

257. Haya ee Moyo Wangu

265. Mganga Wetu ni Karibu